Barabara zote zinazoelekea katika Haram ya Imam Ridha (AS), Imam wa nane wa Waislamu wa Kishia, katika mji mtakatifu alikozikwa wa Mash'had, kaskazini mashariki mwa nchi, zimejaa umati wa waombolezaji waliovalia mavazi meusi na waliofika huko kutoka pembe zote za nchi na maeneo mengine ya dunia kwa ajili ya kuomboleza kifo cha mtukufu huyo wa Nyumba ya Mtume (SAW).
Katika usiku wa kuamkia leo, wananchi Waislamu wa Iran walikusanyika Misikitini na katika maeneo mengine ya ibada na marasimu ya kidini, na hasa katika kaburi lake huko Mash'had, kwa madhumini ya kutoa heshima zao na kumuomboleza mtukufu huyo, mjukuu wa Mtume (SAW).
Imam Ridha (AS) alizaliwa katika mji wa Madina nchini Saudi Arabia mwaka 148 Hijiria na kuuawa shahidi katika siku ya mwisho ya mwezi wa Safar mwaka 203 Hijiria.
Imam Ridha (AS) aliishi katika kipindi ambacho watu walikuwa na hamu kubwa ya kuwajua Watu wa Nyumba ya Mtume na kizazi chake kitoharifu (AS) na kuimarika nafasi yao miongoni mwa watu.
Kwa kuhisi hatari kutokana na mapenzi na uungaji mkono huo mkubwa wa watu kwa Ahlul Bait wa Mtume (SAW) Ma'mun, mtawala wa Bani Abbas katika kipindi hicho, alipanga njama ya kumpa sumu na kumuua Imam (AS).
chanzo: parstoday